Tuesday, October 31, 2017

Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ajivua Ubunge; ajitoa CCM na kuomba kujiunga CHADEMA



NIMEAMUA kujiuzulu NAFASI yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017. HALIKADHALIKA, asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai, Mb., barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya UBUNGE wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa.

AIDHA, Nimechukua UAMZI huo kutokana na kutorishwa kwangu na mwenendo wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa HAKI za Kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya MIHIMILI ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana KIKATIBA.

VILEVILE, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.

MIMI Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA, kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali. AIDHA, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa TAIFA MWALIMU Julius Kambarage Nyerere.

HIVYOBASI, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na haki ya KIKATIBA, natangaza KUKIHAMA Chama Cha Mapinduzi CCM


HISTORIA YAKE:

Lazaro Nyalandu alizaliwa Agosti 18, 1970 mkoani Singida.

Nyalandu alipata elimu ya msingi katika shule za Pohama na Mrumba zilizoko kijijini kwao huko mkoani Singida na kuhitimu mwaka 1987. Aliendelea na masomo ya kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari Kibaha mkoani Pwani (1988 – 1991) na alifaulu vizuri na kujiunga na Shule ya Sekondari Ilboru ambako alisoma kidato cha tano na sita.

Wakati akiwa mwanafunzi wa sekondari, Nyalandu alikuwa kiongozi wa juu wa Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (Ukwata) 1991 – 1993 na baadaye alikuwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania walioteuliwa kuzuru jiji la Rio De Janeiro, Brazil na kushuhudia mkutano wa Mazingira mwaka 1993.

Nyalandu alipata elimu yake ya Chuo Kikuu nchini Marekani ambako alihitimu Shahada ya kwanza ya Sanaa katika Usimamizi wa Biashara (BBA) mwaka 1997 katika Chuo Kikuu cha Wartburg.

Kabla ya hapo alikuwa amepata Shahada ya Biashara ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Wardorf nchini humo. Kiongozi huyu, sasa ana Shahada ya Uzamili aliyoipata kwa njia ya utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Buckingham, Uingereza akifuzu katika masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa na Diplomasia.

Baada ya kuhitimu masomo yake ughaibuni, Nyalandu alianza kazi huko huko Marekani katika Benki ya North West, akifanya kazi katika kitengo cha operesheni za kibenki kati ya mwaka 1998–1999.

Aliporejea nchini Tanzania alifanikiwa kuwa sehemu ya washauri wa mke wa aliyekuwa Rais Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa, katika uendeshaji wa taasisi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).

Ushauri wa timu yake ulisaidia taasisi hiyo kupata misaada mingi kutoka nchi za Ulaya, Marekani, China na nyinginezo. Pia, alikuwa anamsaidia mama huyo katika uandishi wa hotuba zake pale alipokuwa na majukumu makubwa ya kitaifa na kimataifa.

Nyalandu amemwoa mrembo wa Tanzania mwaka 2004 ‘Miss Tanzania’, Faraja Kotta na wana watoto wawili, Sarah na Christopher.

MBIO ZA UBUNGE:

Tangu alipokuwa kijana mdogo, Nyalandu alionyesha kila dalili kuwa na nyota ya uongozi. Watu wanaomfahamu hawakushangaa walipomwona mwaka 2000 anaingia kwenye mpambano ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akilisaka jimbo la Singida Kaskazini. Kutokana na udhaifu wa upinzani uliokuwepo wakati huo alijua atakuwa na kazi kubwa ndani ya chama chake tu, hivyo, alipopitishwa na CCM akapambana majukwaani na wapinzani na kuwa mbunge.

Mwaka 2005, Nyalandu alipitishwa tena na chama chake kuwania ubunge Singida Kaskazini, akakutana tena na upinzani dhaifu kutoka kwa Kimia Omari Rashid wa Chadema, akajivunia asilimia 93.5 ya kura zote na kuwa mbunge hadi mwaka 2010.

Baada ya kupata uzoefu wa ubunge, kwa miaka kumi, Nyalandu alirudi tena kutetea mara ya tatu; CCM ikampa nafasi mwaka 2010 na wananchi wakamchagua kwa ushindi wa asilimia 87.7 akimshinda kwa mara nyingine mgombea yuleyule wa Chadema wa mwaka 2005.

Ushindi wa mara hii ulikuja na bahati kubwa kwa Nyalandu. Bahati ya kwanza ilikuwa kukwea ngazi zaidi. Rais Jakaya Kikwete alimteua Nyalandu kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Novemba 2010 na alidumu hapo hadi Mei 2011 alipohamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii, nafasi aliyokaa kwa takriban miaka mitatu.

Bahati ya pili, Januari 2014, nyota yake ilipaa zaidi akapewa wadhifa mkubwa; mara hii akiteuliwa kuwa waziri kamili wa Maliasili na Utalii, sekta ambayo ina changamoto kubwa sana hapa nchini na sekta hiyo nyeti ambayo imenufaisha mamia ya nchi duniani huku Tanzania watu wengi wakisema utalii haujalisaidia taifa kwa kiasi kinachofaa.

MBIO ZA URAIS:

Nyalandu aliweka wazi nia yake ya kuwania urais Desemba 28, 2014 na alitangaza nia hiyo ya kugombea urais katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Ilongero, katika jimbo analoliongoza, Singida Kaskazini, wakati akihutubia mamia ya wananchi.

Katika mkutano huo alisisitiza kuwa “sasa ni zamu ya vijana kuongoza nchi” huku akiwaambia wananchi kuwa safari yake ya ubunge kwa miaka 15 inaanzisha safari nyingine bila kuwaeleza ikiwa bado ana nia na ubunge au la. Aliambatana na mkewe, watoto wake pamoja na wazazi wake.

Kabla ya kutangaza nia ya urais, Nyalandu aliwahi kusikika akisema kuwa “…siwezi kutangaza kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao bila kutumwa na watu” lakini kabla watu wenyewe hawajamtuma aliibuka na kuwaita yeye mwenyewe mkutanoni na kuweka nia yake.

No comments:

Post a Comment