Wednesday, November 8, 2017

KAMBI RASMI YA UPINZANI YALAANI VITENDO VIOVU ALIVYOTENDEWA MNADHIMU MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHE TUNDU LISSU

Kambi rasmi ya upinzani bungeni imelaani na kupinga vitendo viovu alivyotendewa Mnadhimu wa Kambi hiyo, Tundu Lissu, ambaye alinusurika kifo baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma

Lissu ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali moja ya Nairobi, Kenya.

Akiwasilisha bungeni maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni jana kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/2019 kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa kambi hiyo, David Silinde alisema vitendo hivyo vinatakiwa vikemewe kwa uzito unaostahili.

Silinde ambaye ni Mbunge wa Momba (Chadema), alisema vitendo hivyo vikiachwa viendelee bila kukemewa kuna hatari ya kundi linalohisi kuonewa likakosa uvumulivu na hivyo kuathiri amani ya nchi.

“Ingawa miezi miwili sasa imepita tangu Lissu anusurike kifo baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi wakati mkutano wa nane wa bunge ukiwa unaendelea na vikao vyake hapa Dodoma na mpaka sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na serikali juu ya kukamatwa kwa watu waliohusika na tukio hilo.

“Ikiwa polisi wameshindwa kufanya uchunguzi na kuwakamata wahalifu hao ndani ya miezi miwili, Kambi Rasmi ya upinzani bungeni haioni muujiza wowote unaoeweza kutendeka ili watu hao wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria hata kama polisi wataongezewa miezi mingine miwili.

“Tafsiri ya ukimya huo wa serikali ni rahisi, kwamba hakuna dhamira ya dhati wala utayari wa kushughulikia jambo hilo. Hili la kuanza kutuwinda kwa lengo la kutuua, hatuwezi kamwe kulinyamazia,” alisema.

Alisema Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa wito kwa wananchi wote kupaza sauti zao kupinga uonevu na ukandamizaji wa haki, kupinga matukio ya utekaji, utesaji na umwagaji wa damu katika nchi.

No comments:

Post a Comment