Wednesday, December 27, 2017

MBUNGE LIJUALIKALI AKAMATWA NDANI YA MAHAKAMA MOROGORO



By Hamida Shariff, Mwananchi hshariff@mwananchi.co.tz

Mbunge wa jimbo la Kilombero kupitia chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) Peter Lijualikali amekamatwa na maofisa wa polisi muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa kesi yake yenye mashtaka nane likiwemo la kuchoma moto ofisi ya kijiji.

Lijualikali amekamatwa ndani ya mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro na maofisa hao na kupelekwa katika kituo cha polisi mkoa wa Morogoro kwa kile kilichodaiwa na maofisa hao kuwa wanataka kumhoji zaidi.

Wakati Mbunge huyo akikamatwa alionekana kupigwa na butwaa huku akitii amri ya maofisa wa polisi kwa kufanya kila alichotakiwa huku wafuasi wa Chadema wakionekana kulalamika kwa kudai kuwa mbunge huyo hakutendewa haki.

Akizungumzia tukio la kukamatwa kwa mbunge huyo ndani ya viunga vya mahakama wakili wa upande wa utetezi Barthelomeo Tarimo amewatoa hofu ndugu, jamaa na wanachama wa Chadema na kueleza kwamba polisi wana haki ya kumhoji mbunge huyo wakati wowote.

Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Morogoro 2015 kupitia Chadema Dkt. Marcus Albanus amedai kuwa kitendo cha kukamatwa kwa mbunge huyo ndani ya mahakama kinatengeneza hofu kwa raia hususani wapiga kura wa mbunge huyo wa jimbo la Kilombero.

Dk Marcus alidai kuwa kama maafisa wa polisi walipaswa kutengeneza mazingira ya amani na ya heshima ikiwa ni pamoja na kumuita kituoni ili aende kwa miguu yake mwenyewe badala ya kumkamata hadharani.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kwamba mbunge huyo wa Kilombero Peter Lijualikali, Suzani Kiwanga wa jimbo la Mlimba pamoja na washtakiwa wenzao ambao kwa sasa wamefikia 57 walitenda makosa hayo nane Oktoba 26 mwaka huu katika kijiji cha Sofi Wilaya ya Malinyi mkaoni hapa.

Kabla ya kutajwa kwa kesi hiyo jana mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Ivan Msaki, wakili wa Serikali Karistus Kapinga aliwasilisha ombi mahakamani hapo la kuongeza washtakiwa 15 ambao kwa sasa wameunganishwa katika mashtaka hayo na hivyo kufikia washtakiwa 57.

Wakili Kapinga amedai kuwa upelelezi bado haujakamilika hivyo mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 31 itakapotajwa tena huku washtakiwa 15 waliongezwa kwenye hati ya mashtaka wakitakiwa kurudi Januari 3 na kwamba washtakiwa wote wako nje kwa dhamana ya watu wawili kila mmoja watasaini dhamana Sh5 milioni.

No comments:

Post a Comment